Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa mauaji yaliyofanywa katika mji wa Mpeketoni, Pwani ya Kenya hayakufanywa na kundi la wapiganaji wa kiislamu la Al Shabaab.
Kauli ya Rais Kenyatta inakuja siku moja baada ya kundi hilo kukiri kufanya mauaji yaliyotokea Mpeketoni Jumapili usiku na kuua watu zaidi ya 50.
Akitoa hotuba yake ya kitaifa, Rais Kenyatta pia amesema maafisa wa polisi Mpeketoni ambao walifanya uzembe hadi kutokea mashambulizi hayo watashtakiwa.
Al Shabaab lilikiri katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ndilo lilifanya mauaji hayo Jumatatu jioni.
Mauaji zaidi yalifanyika usiku wa kuamkia leo na kuua watu 20 licha ya taarifa ya Al Shabaab kusema kuwa washambuliaji walioshambulia Mpeketoni walikuwa wamerejea salama nchini Somalia.
Uharibifu mkubwa ulishuhudiwa katika mji huo huku washambuliaji wakichoma hoteli na kituo cha polisi pamoja na kuteketeza magari waliyoyatumia kwa usafiri wao.
Kenyatta amesema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanaochochea uhasama miongoni mwa jamii.