Translate to nother language

Wednesday, November 27, 2013

MAJANGA:Hatimaye Serikali yabariki TANESCO kupandisha bei za umeme....Naibu waziri asema "atakayeshindwa kumudu gharama hizo, atumie kibatari..."





Naibu Waziri wa umeme, Mh George Simbachawene, amesema kwamba serikali imekubali TANESCO waongeze gharama za umeme kwa 68% kama walivyokuwa wameomba.
  



Simbachawene ameitoa  kauli hiyo wakati akiongea katika kipindi cha Kumepambazuka kupitia Radio One leo asubuhi. 






Amesema kwamba hata kama TANESCO wakiongeza gharama za umeme hadi kufikia Tsh 800 kwa unit bei hiyo ni nafuu kuliko gharama za kununua mafuta ya taa.

Mh Simbachawene ametahadharisha kwamba kama mtu ataona kwamba gharama za umeme ni kubwa, basi akawashe kibatari au akae gizani.


Source: Jamiiforum  via Kumepambazuka, Radio One

Naibu Waziri wa Nishati atakiwa kuwaomba RADHI wananchi baada ya kuwaambia kuwa atakayeshindwa kumudu gharama mpya za umeme atumie kibatari

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kutoa kauli ya kukatisha tamaa.
 
Simbachawene,  juzi alitoa kauli ya serikali ya kupandisha bei ya umeme kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lilivyoomba hivi karibuni kutaka kuongeza gharama za nishati hiyo kwa asilimia 68.
 
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa hata TANESCO ikiongeza gharama za umeme hadi kufikia sh 800 kwa uniti bado bei hiyo itaendelea kuwa nafuu ukilinganisha na  gharama za kununua mafuta ya taa.
 
Simbachawene alitoa tahadhari kwamba endapo kuna mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari au akae gizani.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kuwa kauli hiyo inaweza kusababisha vurugu kutokana na suala la umeme kumgusa kila Mtanzania.
 
Alisema kuwa hivi sasa viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kuudhi ambazo ni hatari kwa ustawi wa taifa.
 
“Tunakumbuka kauli za kuudhi zinavyozidi kushamiri wakti ule aliyekuwa Waziri wa Fedha Basili Mramba alipowaambia Watanzania wajifunge mikanda kubana matumizi hata ikibidi kula majani watakula, lakini ndege ya rais lazima inunuliwe; akaja Waziri wa Ujenzi John Magufuli aliyewaambia wakazi wa Kigamboni kuwa kama hawawezi kulipa ongezeko la nauli mpya basi wajifunze kupiga mbizi, ili kuvuka kwa kuogelea, wanaporudi vijijini au wazunguke kupitia Kongowe sasa hii ya vibatari!”alisema.
 
Alisema kuwa ni muhimu viongozi wakahakikisha wanatoa kauli zilizo na hekima ili kuepusha migogoro.
 
Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya serikali kupandisha gharama hizo, muathirika mkubwa ni mwananchi wa chini.
 
Alisema kuwa wamiliki wa viwanda wanachoangalia ni faida hivyo kupanda kwa bei ya umeme kutasababisha gharama za bidhaa kuzidi kuwa juu zaidi.
 
“Nchi za wenzetu hakuna jambo linaloweza kufanywa bila kushirikisha wananchi lakini hapa kwetu wanaamua tu na mbaya zaidi wanakuja na kauli za kuudhi na kukatisha tamaa kwa kuwa Watanzania ni wapole,” alisema.
 
Dk. Bisimba alisema kuwa ni lazima wafahamu kuwa upole wa Watanzania utafikia kikomo na hiyo inaweza kusababisha hatari kwa taifa.
 
Wiki hii wadau mbalimbali wa umeme likiwamo Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), walipinga maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya kuongeza gharama za umeme kwa asilimia 67.8.
 
Walisema ongezeko hilo ambalo limelenga zaidi viwanda vikubwa na vya kati litasababisha kupanda kwa bei za bidhaa za viwandani.
 
Mjumbe wa Bodi ya CTI, Samuel Nyantahe, alisema kabla TANESCO haijapandisha gharama hizo ingekusanya madeni yote na kuziba mianya ya wizi wa umeme.
 
Naye Mjumbe wa CCC Thomas Mnunguli, alisema ongezeko hilo ni kubwa na linakosa uhalali hivyo TANESCO ijitathmini na kujipanga upya na ilenge kutoa huduma bora na nafuu.



Saturday, October 26, 2013

Dr. Mwakyembe Acharuka, Alia na TRA Bandarini
 
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DK. MWAKYEMBE ACHARUKA, ALIA NA TRA BANDARINI
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa ni kikwazo kwake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Dk. Mwakyembe alisema watu wengi wanaoitumia bandari ya Dar es Salaam (TPA) wanalalamikia  madudu wanayofanya TRA hasa  tatizo la kufeli  kwa mfumo wa mawasiliano ya kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.
Alitoa shutuma hizo baada ya kutakiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.
Jana usiku (Alhamisi, Oktoba 24, 2013)Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake ya China kwa kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo maarufu  kwa biashara.
Bw. Stanley Mwakipesile ambaye ni mfanyabiashara wa  Kariakoo anayefuata bidhaa zake katika jimbo la Guangzhou,  katika hoja zake alisema utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na TRA kutofanya kazi siku zingine na hivyo kusababisha mteja kutozwa fedha nyingi.
Mfanyabiasahra huyo alisema kutokana na kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia bandari hiyo na sasa wanatumia bandari ya Mombasa jambo ambalo alisema ni hasara kwa nchi. “Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna urasimu mwingi tu pale lakini cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini mteja anatozwa eti kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.
Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za mfanyabiashara huyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo linalolalamikiwa sana ni TRA ni kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo kutofanya kazi (system down).
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli TRA ni tatizo,  hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza watu wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua tatizo hili,” alisema Mwakyembe.
Alisema licha ya kuwepo agizo kutoka serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji  wa TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu  na wanalala kwa siku 10 katika mwezi mzima.
Alisema wakati TRA wanaenda kulala, mteja hahudumiwi  na wanapokuja kuendelea na kazi kesho yake,  wanawatoza  wateja tozo ya kuchelewesha mzigo wakati makosa siyo ya wateja  bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi kwa Tanzania.
“Sisi TPA hatulali; lakini wenzetu hawa wanalala, inakuwaje wanaenda kulala wakati mizigo imerundikana pale bandarini? Kwa kweli hawa watu ni lazima tushughulike nao.
“Mimi nimesaini BRN, Rais anataka kuona mwaka 2015 shehena inaongezeka pale, na kufikia tani 18 sasa yule atakayekaa mbele yangu kunikwamisha mie nitampitia,” alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa kwa nguvu na watanzania hao.
Hata hivyo aliwatoa hofu Watanzania kwa bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kila mwaka shehena imekuwa inaongezeka, hali inayoonyesha kuwa batu nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe bado zinatumia bandari hiyo.
 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 25, 2013

Monday, October 21, 2013

Usafiri wa Treni wasitishwa kwa muda Dar es Salaam hii leo

 
 Kutokamilika kwa ukarabati wa vichwa vya gari moshi katika karakana ya Morogoro ambalo linatoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam ni miongoni mwa sababu ambayo imetajwa na uongozi wa kampuni ya reli Tanzania (TRL) kusitisha huduma kuanzia leo jumatatu.
Kulingana na taarifa ambayo imetolewa na ofisi ya uhusiano wa kampuni hiyo zimebainisha kuwa ukarabati wa vichwa hivyo utakamilika mapema tarehe 22 na kuwasili jioni kwa lengo la kuendelea kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi kupitia stesheni ya ubungo maziwa hadi stesheni ya dar es salaam
 

Friday, October 18, 2013

Mwanzilishi wa Facebook Zuckerberg anunua nyumba zote za jirani zake,ni baada ya kusikia kuna mtu anataka kukaa karibu nae ili ajitangaze

Inawezekana mwanzilishi na C.E.O wa facebook Mark Zuckerberg anahitaji faragha ya aina yake au hataki usumbufu wa jirani yeyote karibu nae, kwa kuwa ana pesa ya kutosha kufanya yake ameitumia kuwafukuza majirani zake katika eneo hilo, hasa aliposikia kuna mtu anataka kukaa karibu nae ili ajitangaze!
Ripoti zilizotelewa na gazeti la The San Jose Mercury News zimedai kuwa chanzo kimoja ambacho hakikutaka kutajwa kililiambia gazeti hilo kuwa Zuckerberg alisikia kuna mtu aliyetaka kununua sehemu ya eneo hilo kwa lengo la kukaa karibu nae ili baadae atangaze kuwa anaishi karibu na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa facebook.
Hali iliyomfanya Zuckerberg kutoa $30 million na kununua eneo lenye nyumba nne zilizo karibu na nyumba yake iliyoko Palo aloto, Calfornia.

Friday, October 11, 2013

›Wizara ya ujenzi yaagizwa kuendelea na utaratibu wa zamani kwa mwezi mmoja.

Waziri mkuu Mh. Mizengo Pinda ameiagiza wizara ya ujenzi kuendelea na utaratibu wa zamani uliokuwa unatumika kwa wasafirishaji wa malori na mabasi kwa kipindi cha mwezi mmoja wakati serikali ikitafuta ufumbuzi wa kudumu ili kunusuru uchumi wa nchi na ikilazimika mabadiliko ya kanuni yafanyike kwani nazo zinaonekana zina mgogoro.

Mh pinda amelazimika kutoa uamuzi huo jijini Dar es Salaam kufuatia mgomo wa malori uliosababisha baadhi ya shughuli kusimama hasa bandarini ambapo amesema serikali itaunda timu itakayoshirikisha wadau wa usafirishaji pamoja na wizara zenye dhamana ili waweze kuchanganua malalamiko kadhaa yaliyowasilishwa kwake na wasafirishaji hao na mwisho wa siku muafaka uweze kupatikana.
Aidha waziri mkuu hakusita kuzunguimzia suala la ushirikishwaji wa wadau pamoja na suala la rushwa katika mizani ambapo amesema ni tatizo kubwa na kuiagiza Tanroads kuhakikisha inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwani baadhi ya watumishi wa mizani siyo waaminifu pamoja na kuwa wameajiri wengine wapya huku akiitaka wizara ya ujenzi na Tanroads kutengeneza utaratibu ambao siyo lazima magari yote kwa kipindi hiki kupima Kibaha ili kuepuka msongamano ambao unaweza kujitokeza baada ya malori kuanza kazi.
Katika bandari ya Dar es Salaam hali imeendelea kuwa mbaya kutokana na msongamano wa meli zilizopo nje ya bandari ambazo zinasubiri kupakua mizigo ambapo imeshuhudiwa baadhi ya mizigo ambayo ilitakiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi ikiwa imehifadhiwa eneo la dharura na mamlaka ya bandari huku kaimu meneja wa mawasiliano wa mamlaka ya bandari Tanzania TPA Bi Janeth Ruzangi akielezea athari zilizotokana na mgomo huo.
Mgomo huo ulioingia siku ya sita ulianza Octoba tano mwaka huu huko eneo la mizani Kibaha na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro baada ya wasafirishaji hao kutakiwa kutoa tozo ya asilimia tano ya uzito unaozidi ambapo mbali na kudhorotesha shughuli za bandari pia umesababisha upungufu wa mazao ya nafaka katika masoko ya jiji baada ya malori mengi kushindwa kusafiri kutoka mikoani.